Jumatatu 23 Novemba 2026 - 10:54
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rafii Aelezea Sifa Tano Muhimu za Mtukufu Ummul-Banin (sa)

Hawza/ Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rafii, akifafanua vipengele mbalimbali vya maisha na tabia za Mtukufu Ummul-Banin (sa), ametaja sifa tano muhimu zilizomtambulisha mwanamke huyo mtukufu, ambazo ni kujitolea, adabu, subira, ushujaa na uaminifu. Aidha, akieleza kuwa Mtukufu Ummul-Banin (sa) alijitolea wanawe wote wanne katika njia ya Imam Hussein (as), amesema kuwa maisha ya mwanamke huyo ni mfano wa kudumu wa imani na kujitolea.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza kutoka Tehran, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Nasir Rafii, siku ya Jumapili, katika kipindi cha televisheni cha «Samt-e Khoda» (Kumuelekea Mwenyezi Mungu), akizungumzia nafasi ya Ummul-Banin (sa) katika familia ya Amirul-Muuminina Ali (as), alisema: Mwanamke huyo mtukufu, baada ya kuuawa kishahidi Bibi Fatimah Zahraa (sa), alichukua jukumu la kuwasimamia na kuwalea watoto wadogo wa Imam Ali (as). Wakati huo, watoto wa Bibi Fatimah Zahraa (sa) walikuwa wamekua na tayari walikuwa na maisha yao ya kujitegemea, lakini watoto wa Bibi Ummul-Banin (sa) walikuwa bado wadogo. Baada ya Imam Ali (as) kuuawa kishahidi, watoto hao pia walimpoteza baba yao.

Aliongeza kuwa, baada ya kuuawa kishahidi Amirul-Muuminina Ali (as), Bibi Ummul-Banin (sa) aliwalea watoto wake wanne katika mazingira magumu bila uwepo wa baba yao. Jambo hili linapata umuhimu mkubwa zaidi tunapofahamu kuwa, katika tukio la Karbala, licha ya kufahamu hatari za safari hiyo na uwezekano wa Imam Hussein (as) kuuawa kishahidi, aliwasindikiza wanawe wote wanne waandamane na Imam Hussein (as).

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rafii, akieleza kuwa; baadhi ya watu katika mazingira kama hayo wangeweza kuacha mtoto mmoja au kadhaa nyumbani ili wabaki nao, alisema: Bibi Ummul-Banin (sa) alijitolea watoto wake wote katika njia ya kuambatana na Imam Hussein (as). Kitendo hiki kinaonesha sifa ya kwanza na ya wazi ya mwanamke huyo mtukufu, nayo ni kujitolea. Kujitolea kunapata maana yake halisi pale mwanadamu anapokuwa tayari kuacha kila kitu alichonacho kwa ajili ya lengo kubwa zaidi.

Mwalimu huyo wa Hawza na chuo kikuu aliitaja Adabu kuwa sifa ya pili ya Bibi Ummul-Banin (sa), akizungumzia namna alivyopokea taarifa za kuuawa kishahidi wanawe, alisema: Katika baadhi ya riwaya zilizosimuliwa kutoka kwa mwanamke huyo mtukufu, imeelezwa kuwa baada ya kupokea taarifa za kuuawa kishahidi wanawe, aliulizia kwanza hali ya Imam Hussein (as), kisha akasema: «Wanawe na kila kilichopo chini ya mbingu viwe fidia kwa Hussein (as).»

Kauli hii inaonesha kiwango cha juu cha adabu na utambuzi wake kuhusu nafasi na hadhi ya Imam Hussein (as).

Aliendelea kusema kuwa, hakuna malalamiko au manung’uniko yaliyosimuliwa kutoka kwa mwanamke huyo mtukufu kutokana na kuuawa kishahidi wanawe wote wanne, ilhali kupoteza watoto wanne ni jambo gumu mno kwa mama yeyote. Hata katika mazingira hayo, Bibi Ummul-Banin (sa) aliendelea kuzingatia nafasi ya Imam na lengo ambalo wanawe walikuwa wamejitolea maisha yao kwa ajili yake.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rafii alitaja Subira na uvumilivu kuwa sifa ya tatu ya mwanamke huyo mtukufu, akisema: Fikirieni mama ambaye ameishi na watoto wake wanne kwa miaka mingi na kuwalea hadi wakakua, lakini mwishowe anawapoteza wote wanne. Kuvumilia msiba wa namna hiyo ni jambo gumu sana, na Bibi Ummul-Banin (sa) ni mfano mashuhuri wa subira wakati wa kukumbwa na misiba.

Akirejelea Aya isemayo:

«وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُمْ مُصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ»

“Na wape bishara njema wenye kusubiri; ambao wanapopatwa na msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na hakika kwake Yeye tutarejea.”

Aliongeza kuwa subira wakati wa misiba ni miongoni mwa sifa zenye thamani kubwa kwa waumini, na maisha ya Bibi Ummul-Banin (sa) yanaonesha mfano ulio wazi wa sifa hiyo.

Mtaalamu huyo wa masuala ya dini aliutaja Ushujaa kuwa sifa ya nne ya Bibi Ummul-Banin (sa), huku akizungumzia ushujaa uliooneshwa na wanawe katika tukio la Karbala, alisema: Ushujaa ulioonekana katika tabia na matendo ya wanawe una uhusiano pia na nafasi ya malezi ya mama yao. Mtukufu Abul-Fadhl Abbas (as) ni mfano wa wazi wa ushujaa huo; alikuwa mtu ambaye maadui walishindwa kustahimili ushujaa wake katika uwanja wa mapambano.

Akizungumzia uwepo wa Mtukufu Abbas (as) katika eneo la mto Furati na makabiliano yake na jeshi la maadui, alisema kuwa katika baadhi ya mapokezi imeelezwa kwamba, kutokana na mashambulizi ya Mtukufu Abbas (as), watu wengi kutoka katika jeshi la upande wa pili walitawanyika.

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rafii pia alizungumzia uaminifu wa Mtukufu Abbas (as), akiongeza kuwa sifa hiyo imesisitizwa pia katika Ziyara yake. Uaminifu huo, sambamba na ushujaa, ni miongoni mwa sifa zake mashuhuri.

Aidha, akiashiria nafasi ya kiroho ya Bibi Ummul-Banin (sa) na namna watu wanavyomwelekea kwa njia ya Tawassul, alisema: Watu wengi wanapokumbwa na shida na matatizo mbalimbali, humuelekea Bibi Ummul-Banin (sa) kwa njia ya kutawassali kupitia yeye. Kitendo hiki cha Tawassul kina nafasi ya pekee miongoni mwa wapenzi wa Ahlul-Bayt (as).

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rafii Aelezea Sifa Tano Muhimu za Mtukufu Ummul-Banin (sa)

Hujjatul-Islam wal-Muslimin Rafii

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha